2 Peter 1

1 aSimoni Petro, mtumishi na mtume wa Isa Al-Masihi:

Kwa wale ambao kwa njia ya haki ya Mungu na Mwokozi wetu Isa Al-Masihi mmepokea imani iliyo na thamani kama yetu:

2 bNeema na amani iwe kwenu kwa wingi katika kumjua Mwenyezi Mungu na Isa Bwana wetu.

Wito Wa Mkristo Na Uteule

3 cUweza wake wa uungu umetupatia mambo yote tunayohitaji kwa ajili ya uzima na uchaji wa Mungu, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe. 4 dKwa sababu hiyo, ametukirimia ahadi zake kuu na za thamani kupitia mambo haya, ili kupitia hayo mpate kuwa washiriki wa asili ya uungu, na kuokoka kutoka upotovu ulioko duniani unaosababishwa na tamaa mbaya.

5 eKwa sababu hii hasa, jitahidini sana katika imani yenu kuongeza wema; na katika wema, maarifa; 6 fkatika maarifa, kiasi; katika kiasi, saburi; katika saburi, utauwa;
Maana yake kumcha Mungu.
7 hkatika utauwa, upendano wa ndugu; na katika upendano wa ndugu, upendo. 8 iKwa maana haya yakiwa ndani yenu kwa wingi na kuzidi kuongezeka, yanawasaidia msikose bidii wala kutozaa matunda katika kumjua Bwana wetu Isa Al-Masihi. 9 jLakini mtu yeyote asipokuwa na mambo haya haoni mbali, na ni kipofu, naye amesahau kule kutakaswa kutoka dhambi zake za zamani.

10 kKwa hiyo, ndugu zangu, fanyeni bidii zaidi kuuthibitisha wito wenu na uteule wenu. Kwa maana mkifanya hivyo, hamtajikwaa kamwe, 11 lna mtajaliwa kwa ukarimu mwingi kuingia katika ufalme wa milele wa Bwana na Mwokozi wetu Isa Al-Masihi.

Unabii Wa Maandiko

12 mHivyo nitawakumbusha mambo haya siku zote, hata ingawa mnayajua na mmethibitishwa katika kweli mliyo nayo. 13 nNaona ni vyema kuwakumbusha mambo haya wakati wote niwapo katika hema hili ambalo ni mwili wangu, 14 okwa sababu najua ya kwamba hivi karibuni nitaliweka kando, kama vile Bwana wetu Isa Al-Masihi alivyoliweka wazi kwangu. 15 pNami nitafanya kila juhudi kuona kwamba baada ya kuondoka kwangu mtaweza kuyakumbuka mambo haya siku zote.

16 qTulipowafahamisha juu ya uweza na kuja kwa Bwana wetu Isa Al-Masihi, hatukufuata hadithi zilizotungwa kwa werevu, bali tulishuhudia kwa macho yetu ukuu wake. 17Alipewa heshima na utukufu kutoka kwa Mungu Baba, sauti ilipomjia katika Utukufu Mkuu, ikisema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa. Ninapendezwa naye sana.” 18Sisi wenyewe tuliisikia sauti hii ambayo ilitoka mbinguni, wakati tulipokuwa pamoja naye kwenye ule mlima mtakatifu.

19 rNasi tunalo pia neno la hakika zaidi la unabii, ambalo mtafanya vyema mkiliangalia kwa bidii, kama vile nuru inavyong’aa gizani, hadi kupambazuka na nyota ya asubuhi izuke mioyoni mwenu. 20 sZaidi ya yote, yawapasa mjue kwamba hakuna unabii katika Maandiko uliofasiriwa kama alivyopenda nabii mwenyewe. 21 tKwa maana unabii haukuja kamwe kwa mapenzi ya mwanadamu, bali watu walinena yaliyotoka kwa Mungu wakiongozwa na Roho Mtakatifu.
Copyright information for SwhKC